Waziri Mkuu wa Sudan achelewa kutangaza baraza la mawaziri
Waziri mkuu mpya wa Sudan bado hajatangaza baraza lake jipya la mawaziri pamoja na kuwa alikuwa ametakiwa kuitangaza serikali yake kufikia jumatano.
Waziri Mkuu Abdallah Hamdok, ambaye aliapishwa wiki iliyopita, alikuwa anatazamiwa kutangaza baadhi ya mawaziri muhimu kutoka katika orodha aliyopewa na Harakati ya Uhuru na Mabadiliko (FCC), kundi ambalo lilikuwa mstari wa mbele katika maandamano ya mtaani yaliyouangusha utawala wa miaka 30 wa Omar al Bashir na baada ya hapo kulazimisha baraza la kijeshi lililochukua mamlaka kugawana mdaraka na raia.
Imedokezwa kuwa, tangazo la baraza la mawaziri lilicheleweshwa kwa sababu "majadiliano juu ya uteuzi wa mawaziri bado yanaendelea,"
Serikali mpya ya Sudan inapaswa kuundwa na jumla ya mawaziri 20, walioteuliwa na Bwana Hamdok isipokuwa Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi, ambao watateuliwa na askari wanaojumuika kwenye Baraza Kuu Tawala.
Baada ya kuapishwa, Hamdok amewaambia wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba, kusitishwa vita na kuimarisha amani endelevu ndiyo mahitaji muhimu zaidi katika kipindi kijacho nchini Sudan. Hamdok amesisitiza kuwa baada ya masuala hayo serikali yake itatoa kipaumbele kwa juhudi za kutatua mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoisumbua Sudan na kuongeza kuwa, nchi hiyo ina uwezo wa kupata maendeleo na ustawi wa kiuchumi.