Afrika Kusini yakiri: "Afrophobia" inahusika katika hujuma zinazowalenga raia wa kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55817-afrika_kusini_yakiri_afrophobia_inahusika_katika_hujuma_zinazowalenga_raia_wa_kigeni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuwa tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhdi ya raia wa nchi nyingine za Afrika wanaoishi nchini humo ni moja kati ya sababu za mashambulizi na hujuma zinazowalenga wafanyabiashara wa nchi za kigeni katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2019 08:16 UTC
  • Naledi Pandor
    Naledi Pandor

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuwa tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhdi ya raia wa nchi nyingine za Afrika wanaoishi nchini humo ni moja kati ya sababu za mashambulizi na hujuma zinazowalenga wafanyabiashara wa nchi za kigeni katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Naledi Pandor ametoa matamshi hayo siku moja baada ya Afrika Kusini kufunga ubalozi wake nchini Nigeria ikihofia vitendo vya ghasia na ulipizaji kisasi wa Wanigeria waliokasirishwa na mauaji na hujuma zinazowalenga raia wa nchi za Kiafrika huko Afrika Kusini. Pandor amesema Pretoria imechukua uamuzi wa kufunga kwa muda ubalozi wake mjini Abuja kwa sababu za kiusalama kufuatia maandamano ya Wanigeria wanaopinga hujuma dhidi ya raia wa kigeni huko Afrika Kusini (Xenophobia).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amekiri kwamba kuna chuki dhidi ya raia wa mataifa mengine ya Afrika "Afrophobia" na kuna haja ya suala hilo kushughulikiwa. "Siwezi kukanusha kwamba Waafrika kutoka maeneo mbalimbali ya bara hili wanashambuliwa lakini pia kuna uhalifu", amesisitiza Naledi Pandor.

Machafuko na hujuma zinazowalenga raia wa nchi za Kiafrika nchini Afrika Kusini zimeghubika na kuathiri Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika mjini Cape Town. Nigeria imesusia mkutano huo kutokana na hujuma zinazowalenga Waafrika ambazo wiki hii pekee zimesababisha mauaji ya watu wasiopungua 5.

Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo, leo Alkhamisi alitazamiwa kuhutubia sehemu ya mkutano huo juu ya biashara ya nishati duniani.

Nigeria pia imetangaza kuwa itatoa huduma ya bure ya usafiri wa ndege za kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo walioko Afrika Kusini. Huduma hiyo itaanza Jumamosi ijayo.