Serikali mpya ya Sudan yaahidi kuwashughulikia mafisadi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55846-serikali_mpya_ya_sudan_yaahidi_kuwashughulikia_mafisadi
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan ameahidi kwamba, serikali yake itawashtaki na kuwapandisha kizimbani mafisadi wote na kwamba, haitakuwa na huruma katika hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2019 22:08 UTC
  • Serikali mpya ya Sudan yaahidi kuwashughulikia mafisadi

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan ameahidi kwamba, serikali yake itawashtaki na kuwapandisha kizimbani mafisadi wote na kwamba, haitakuwa na huruma katika hilo.

Abdallah Hamdok ametangaza kuwa, mafisadi wote watashtakiwa na kukabidhiwa kwa vyombo vya sheria na kwamba, itahakikisha mali zote zilizoporwa na waliokuwa katika serikali iliyotangulia zinarejeshwa.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan amesema pia kuwa, hatua inayofuata sasa baada ya kuundwa baraza la mawaziri ni kufanya juhudi za kufanikisha malengo ya mapinduzi.

Serikali ya mpito ya Sudan itafanya kazi chini ya usimamizi wa Baraza la Utawala wa Mpito litnaloongozwa na wajumbe 11 na litaongoza kwa muda wa miaka 3 kuelekea uchaguzi mkuu. 

Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan al-Bashir

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda  baraza la kijeshi.  

Serikali mpya ya Sudan inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kuboresha uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika vibaya, kupambana na ufisadi, na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.