Sep 11, 2019 06:54 UTC
  • Kamisheni ya Haki za Binadamu: Saudia imehusika katika mauaji ya Waislamu Nigeria

Mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao makuu yake mjini London, Uingereza amesema ni mantiki kuhukumu kuwa kulikweko na mkono wa Saudi Arabia katika mauaji ya Waislamu waliokuwa katika maombolezo ya Siku ya Ashura (tarehe 10 Muharram) wakikumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein AS hapo jana nchini Nigeria.

Massoud Shadjareh aliyasema hayo jana jioni katika kipindi cha The Debate cha kanali ya Press TV na kufafanua kuwa, "Ukweli wa mambo ni kuwa, serikali ya Nigeria imeshindwa kudhibiti mambo. Serikali hiyo inadhibitiwa na Saudia ambayo imeimiminia fedha nyingi, kama ilivyofanya huko nyuma kwa viongozi wa Sudan na Malaysia."

Amebainisha kuwa, ukiweka kwenye mizani kauli ya Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia ambaye amekuwa akijipiga kifua na kusema kuwa wameidhibiti serikali ya Nigeria sambamba na kuwazima wapinzani, utafika kwenye mantiki inayohukumu kwamba kuna mkono wa Aal-Saud katika ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria.

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imesema kuwa, askari wa serikali ya Nigeria waliwafyatulia risasi Waislamu walioshiriki katika shughuli ya maombolezo ya Ashura hapo jana na kuua watu wasiopungua 12 na kujeruhi makumi ya wengine.

Waislamu wa Nigeria wakiwabeba majeruhi wa hujuma za maafisa usalama

Hii si mara ya kwanza kwa askari wa Nigeria kushambulia umati wa Waislamu wakishiriki katika shughuli ya maombolezo na kukumbuka mauaji ya Imam Hussein (AS).

Mwaka jana pia jeshi la Nigeria lilishambulia mjumuiko mkubwa wa Waislamu walioshiriki maombolezo ya siku ya Ashura katika mji wa Zaria huko kaskazini mwa Nigeria na kuua shahidi watu kadhaa. 

Tags