Baraza la Utawala Sudan na waasi kufanya mazungumzo
Mazungumzo ya amani baina ya Baraza la Utawala nchini Sudan na makundi ya waasi yamepangwa kuanza Oktoba 14 hadi mwezi Disemba ili kurejesha utulivu nchini humo.
Tangazo hilo lilitolewa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika mjini Juba, Sudan Kusini kati ya wawakilishi wa Baraza la Utawala la Sudan na makundi ya waasi na wapiganaji yanayotoka majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile. Mazungumzo ya pande hizo mbili yalifanyika Septemba 11 kufuatia pendekezo la upatanishi lililotolewa na Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini.
Pande hizo pia zimeafiki kuunda kamati maalumu za kupanga mazungumzo ya amani, kufuatilia utaratibu wa kuwaachia huru wahalifu wa kivita na wafungwa, kushughulikia hatua za kumaliza uhasama na kuidhinisha utaratibu wa usimamizi.
Hayo yanajiri siku chache baada ya serikali mpya kuapishwa nchini Sudan likiwa ni baraza la kwanza la mawaziri tangu Rais wa zamani wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir aondolewe madarakani Aprili mwaka huu.

Baraza jipya la mawaziri nchini Sudan linaloongozwa na Waziri Mkuu Abdallah Hamdok lina mawaziri 18 wakiwemo wanawake wanne.
Serikali mpya ya Sudan inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kuboresha uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika vibaya, kupambana na ufisadi, na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kurejesha amani katika maeno yote ya nchi hiyo.