Sep 12, 2019 11:52 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram waua wanajeshi 9 wa Nigeria

Magaidi wa kundi la Boko Haram wameshambulia kituo cha kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuwaua wanajeshi tisa.

Duru zinadokeza kuwa magaidi hao wakufurishaji walishambulia kituo cha Jeshi Jumanne katika mji wa Gudumbali, katika jimbo la Borno ambalo ni ngome ya magaidi hao wa Boko Haram.

Taarifa zaidi zinasema mbali na wanajeshi tisa kupoteza maisha katika hujuma hiyo, wengine 27 hawajulikani waliko.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria Sagir Musa amethibitisha kutokea shambulizi hilo lakini hakutaja idadi ya wanajeshi waliouawa au kutoweka.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.

Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi jambo ambalo limepelekea liendelee kutekeleza mashambulizi yake.

Tags