Somaliland yasimamisha ujenzi wa kituo cha kijeshi cha Imarati
Serikali ya eneo lenye utawala wa ndani la Somaliland nchini Somalia limesimamisha ujenzi wa Umoja wa Falme za Kiarabu wa kituo chake cha kijeshi katika bandari ya Berbera.
Muse Bihi Abdi, Rais wa eneo hilo ametoa tangazo hilo kupitia njia ya televisheni na kuongeza kuwa, "Uwanja wa ndege wenye utata na ambao ulikuwa unakarabatiwa na UAE, sasa umebadilishwa na kuwa uwanja wa kiraia."
Amesema kuanzia wiki ijayo, uwanja huo wa kijeshi utaendelea kukarabatiwa na kampuni tofauti, na haupo tena mikononi mwa Imarati.
Mwaka jana, Abukar Dahir Osman, Mwakilishi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa alilaani ujenzi huo wa Umoja wa Falme za Kiarabu akisisitiza kuwa unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kutaka hatua za lazima zichukuliwe ili kusitisha ujenzi huo.
Serikali ya Mogadishu imeyataja makubaliano kati ya Imarati na eneo la Somaliland juu ya ujenzi huo kuwa ni kinyume cha sheria na ni uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na ardhi nzima ya Somalia.
Mpango huo wa Imarati wa kutaka kujenga kambi yake ya kijeshi huko Somaliland ulipingwa vikali pia na nchi jirani zikiwemo Ethiopia na Djibouti.