Sudan yaunda kamati ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji ya waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56186-sudan_yaunda_kamati_ya_kutafuta_ukweli_kuhusu_mauaji_ya_waandamanaji
Waziri Mkuu wa Sudan ametoa agizo la kuundwa kamati maalumu ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji dhidi ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama Juni mwaka huu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 23, 2019 03:42 UTC
  • Sudan yaunda kamati ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji ya waandamanaji

Waziri Mkuu wa Sudan ametoa agizo la kuundwa kamati maalumu ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji dhidi ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama Juni mwaka huu.

Abdallah Hamdok, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan amesema kuwa, kuna haja ya kuundwa haraka kamati hiyo na kufuatilia faili la mauaji dhidi ya makumi ya waandamanaji.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kamati hiyo itajumuisha watu saba na itaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, wajumbe kutoka Wizara za Sheria, Ulinzi na Mambo ya Ndani pamoja na watu wengine watatu wasiofungamana na serikali.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Sudan imesema kuwa, kamati hiyo itakuwa na muda wa miezi mitatu kukamilisha jukumu hilo na endapo kutakuwa na haja itaongezewa muda.

Mawaziri wa Serikali ya Mpito ya Sudan wakila kiapo

Tume hiyo itapaswa kufanya kazi zake kwa uhuru kamili na kutoingiliwa na asasi za serikali au za kisheria.

Makumi ya raia waliuawa Juni 3 mwaka huu mbele ya makao makuu ya vikosi vya ulinzi mjini Khartoum, baada ya vyombo vya usalama kuwafatulia risasi hai waandamanaji waliokuwa wakitaka kuweko utawala wa kiraia katika nchi yao baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir. 

Baadhi ya duru zinasema watu wasiopungua 128 waliuawa katika sokomoko hilo, na wananchi wa Sudan wanalituhumu Baraza la Mpito la wakati huo, kwamba, ndilo lililohusika na mauaji hayo.