Abdalla Hamdok asisitiza kuhitimishwa vurugu za ndani nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56304-abdalla_hamdok_asisitiza_kuhitimishwa_vurugu_za_ndani_nchini_sudan
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan amesema kuwa, serikali yake inatoa kipaumbele juu ya suala la kuhitimishwa vurugu na machafuko ya ndani nchini humo na kuandaa mazingira mazuri ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 28, 2019 23:01 UTC
  • Abdalla Hamdok asisitiza kuhitimishwa vurugu za ndani nchini Sudan

Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan amesema kuwa, serikali yake inatoa kipaumbele juu ya suala la kuhitimishwa vurugu na machafuko ya ndani nchini humo na kuandaa mazingira mazuri ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Abdalla Hamdok amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa pambizoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kueleza kwamba, sambamba na kuhakikisha kuwa, kunakuweko uhusiano mzuri baina ya nchi hiyo na jirani yake Sudan Kusini, serikali yake inalipa umuhimu maalumu suala la kuhitimishwa vurugu na machafuko ya ndani na kuweka nguzo imara kwa ajili ya kuweko amani ya kudumu katika nchi hiyo.

Abdalla Hamdok amesema pia, serikali ya sasa ya Khartoum inakaribisha kwa mikono miwili juhudi za kuimarishwa uhusiano na Sudan Kusini sambamba na kuboresha maisha ya wananchi.

Baraza jipya la mawaziri nchini Sudan likila kiapo cha utiifu

Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali mpya ya Sudan inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kuboresha uchumi wa nchi hiyo uliosambaratika vibaya, kupambana na ufisadi, na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir. Hatimaye baada ya vuta nikuvute hatimaye nchini Sudan kumeundwa serikali ya mpito itakayoongoza kwa kipindi cha miaka mitatu kuelekea uchaguzi mkuu.