Maafisa wa utawala uliopinduliwa Sudan wafutwa kazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56428-maafisa_wa_utawala_uliopinduliwa_sudan_wafutwa_kazi
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan amewafuta kazi maafisa 67 wa serikali ambao wanafungamana na utawala uliopinduliwa wa Omar al Bashir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2019 03:18 UTC
  • Maafisa wa utawala uliopinduliwa Sudan wafutwa kazi

Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan amewafuta kazi maafisa 67 wa serikali ambao wanafungamana na utawala uliopinduliwa wa Omar al Bashir.

Kwa mujibu wa gazeti la Sudan Tribune, maafisa wote wa serikali waliofutwa kazi walikuwa na uhusiano wa karibu na utawala wa al Bashir na miongoni mwa waliotimuliwa ni Kansela wa Chuo Kikuu cha Khartoum, waziri mkuu wa zamani Mohammad Tahir Ayla na waziri wa zamani wa mambo ya nje  Ibrahim Gandou.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdullah Hamdouk amefafanua kuhusu kufutwa kazi maafisa hao na kusema analenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika mfumo wa kiidara sambamba na kupambana na ufisadi.

Abdallah Hamdouk aliapishwa Agosti kuwa Waziri Mkuu mpya wa serikali ya mpito ya Sudan. Kuapishwa kwake kulihitimisha machafuko ya miezi kadhaa nchini Sudan yaliyoanza kabla ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir na kuendelea kwa mauaji ya mamia ya raia wa nchi hiyo baada ya kiongozi huyo kupinduliwa na jeshi Aprili mwaka huu.   

Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir akiwa kizimbani

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili lilimpindua madarakani rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda  baraza la kijeshi na hatimaye kuafikia kuundwa serikali ya mpito.