Mazungumzo ya serikali ya Sudan na waasi yaanza Juba
Wawakilishi wa serikali ya Sudan na viongozi wa makundi ya waasi wanaendeleza mazungumzo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
Mazungumzo hayo ya amani yameanza kufuatia mwito wa nchi za eneo kwa pande hizo kuonyesha nia ya kisiasa ya kutatua mgogoro ambao umekuwa ukitokota nchini humo kwa muda mrefu.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini anasimamia mazungumzo kati ya serikali ya mpito ya Sudan na makundi ya waasi.
Kiir amesema mazungumzo hayo ni matokeo ya ahadi ya Sudan Kusini kuhusu kuendeleza juhudi kwa ajili ya kurudisha amani na utulivu katika eneo hilo.
Rais Kiir amezitaka pande mbalimbali za mazungumzo hayo zioneshe nia ya kisiasa na kufikia maelewano kwa ajili ya kutimiza amani na ustawi kwa wananchi wa Sudan.
Mazungumzo hayo yalianza rasmi Jumatatu kati ya Khartoum na waasi wa majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile.
Sudan imejipa miezi sita kufikia mkataba kamili wa amani. Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdallah Hamdok amesema kupata amani ya kudumu ni kipaumbele cha serikali anayoiongoza. Mazungumzo ya Juba yametajwa kuwa hatua ya kwanza katika mazungumzo ambayo yanapaswa kufikia amani kamili ya kudumu nchini Sudani.