Sudan yasema waasi wa Darfur wamekiuka mapatano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56760-sudan_yasema_waasi_wa_darfur_wamekiuka_mapatano_ya_amani
Jeshi la Sudan limesema kundi la waasi la SLM limekiuka mapatano ya kusitisha vita yaliyotangazwa baina ya pande hasimu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 21, 2019 04:45 UTC
  • Sudan yasema waasi wa Darfur wamekiuka mapatano ya amani

Jeshi la Sudan limesema kundi la waasi la SLM limekiuka mapatano ya kusitisha vita yaliyotangazwa baina ya pande hasimu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Sudan inasema kundi la SLM linaloongozwa na Abdul-Wahid Nur limeshambulia jeshi la serikali katika eneo la Brobas, kilomita 8 kutoka eneo la Kara huko Darfur. Taarifa jiyo imeongeza kuwa jeshi la serikali lilijibu mashambulizi na kuwafukuza washambuliaji.

Hata hivyo jeshi la Sudan limesema litaendelea kufuata makubaliano ya kusimamisha vita liliyoyatangaza hivi karibuni, na kusema limeonesha nia njema kwa kuwaachia huru wafungwa 21 wanachama wa kundi la SLM linaloongozwa na Bw Abdul-Wahid.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdallah Hamdok

Hayo yanajiri wakati ambao wiki iliyopita wawakilishi wa serikali ya Sudan na viongozi wa makundi ya waasi walianza mazungumzo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.

Mazungumzo hayo ya amani yanafanyika kufuatia mwito wa nchi za eneo kwa pande hizo kuonyesha nia ya kisiasa ya kutatua mgogoro ambao umekuwa ukitokota nchini humo kwa muda mrefu.

Sudan imejipa miezi sita kufikia mkataba kamili wa amani. Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdallah Hamdok amesema kupata amani ya kudumu ni kipaumbele cha serikali anayoiongoza. Mazungumzo ya Juba yametajwa kuwa hatua ya kwanza katika mazungumzo ambayo yanapaswa kufikia amani kamili ya kudumu nchini Sudan.