Al Bashir abambwa akiwa na simu ya kisasa ndani ya jela Sudan
-
Omar al Bashir
Kugunduliwa simu ya kisasa ya rais aliyeondolewa madarakani na wananchi wa Sudan akiwa katika jela kumezusha malalamiko makubwa nchini humo.
Taarifa zinasema kuwa, Jumuiya ya Kupambana na Ufisadi ya Zero Corruption ndiyo iliyofichua habari ya kukamatwa simu iliyokuwa aikitumiwa na Omar al Bashir akiwa jela.
Jumuiya hiyo imetangaza kuwa, simu ya kisasa (smartphone) ya al Bashir iliingizwa jela ya Kobar anakoshikiliwa rais huyo wa zamani kupitia kwa askari aliyekuwa akifanya kazi katika jela hiyo. Askari huyo ameachishwa kazi lakini ameajiriwa katika taasisi inayomilikiwa na chama cha Omar al Bashir ambako analipwa mshahara mkubwa.
Jumuiya ya Zero Corruption imekosoa uzembe wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Sudan na kushindwa kwake kudhibiti mawasiliano ya Omar al Bashir na wanasaidizi wake wanaoshikiliwa gerezani kwa tuhuma za ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka.
Ripoti zinasema al Bashir amekuwa akiwasiliana na kuwaongoza wafuasi wake akiwa jela kupitia mitandao ya kijamii kama Whats app.
Omar Hassan al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka huu kufuatia maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa ya wananchi. Maandamano hayo yalichochewa na hali mbaya ya uchumi, ufisadi mkubwa na utumiaji mbaya wa madaraka wa al Bashir.