Askari elfu 10 wa Sudan waondoka Yemen
Naibu Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan amesema kuwa askari elfu 10 wa nchi hiyo wameondoka nchini Yemen.
Mohammed Hamdan Dagalo amesema kuwa jehi la Sudan limenza kuondoka hatua hatua nchini Yemen na askari elfu 10 wameondoka nchini humo katika awamu ya kwanza.
Dagalo ameongeza kuwa, hakuna askari wengine watakaoplekwa Yemen kuchukua nafasi za wanajeshi hao elfu kumi waliorejeshwa nyumbani.
Wanajeshi mamluki wa Sudan walitumwa nchini Yemen kushirikiana na Saudi Arabia na Imarati katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa dhidi ya taifa la Yemen wakati wa utawala wa Jenerali Omar al Bashir aliyeondolewa madarakani tarehe 11 mwezi Aprili mwaka huu. Al Bashir alituma jeshi la Sudan kupigana Yemen mkabala wa kupewa pesa kutoka Saudi Arabia.
Kuwepo kwa wanajeshi wa Sudan katika vita vya Yemen kunapingwa sana na makundi ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo hasa baada ya mamia miongoni mwao kuuawa wakipigana kwa niaba ya Saudi Arabia.
Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ikishirikiana na Imarati, Marekani, utawala haramu wa Israel na waitifaki wao iliivamia Yemen na kuanzisha vita vilivyoua maelfu ya raia wasio na hatia. Vita hivyo vinaandamana na mzingiro wa pande zote dhidi ya taifa la Yemen.