Fayez al Sarraj: Mashambulizi ya droni za Imarati hayatasalia bila jibu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58030-fayez_al_sarraj_mashambulizi_ya_droni_za_imarati_hayatasalia_bila_jibu
Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya jana usiku alisema kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) za Imarati katika maeneo ya Zliten na Msalata kaskazini mwa nchi hiyo ni hatua ya kihalifu ambayo haitasalia bila ya jibu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2019 03:23 UTC
  • Fayez al Sarraj: Mashambulizi ya droni za Imarati hayatasalia bila jibu

Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya jana usiku alisema kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) za Imarati katika maeneo ya Zliten na Msalata kaskazini mwa nchi hiyo ni hatua ya kihalifu ambayo haitasalia bila ya jibu.

Droni za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) jana Jumamosi ziliyashambulia maeneno ya Zliten na Msallata kaskazini mwa Libya na kuua watu wasiopungua 3. Imarati ni moja ya nchi waungaji mkono wakuu wa kundi la wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Khalifa Haftar. 

Kundi hilo la wanamgambo chini ya uongozi wa kamanda muasi Haftar ambalo kwa miaka kadhaa sasa linayadhibiti maeneo ya mashariki mwa Libya kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi; miaka kadhaa yakaribuni lilisonga mbele upande wa kaskazini mwa nchi. Kamanda Haftar Aprili Nne mwaka huu aliwaamuru wapiganaji wake kuushambulia mji mkuu Tripoli. 

Kamanda Khalifa Haftar

Shambulio hilo dhidi ya mji mkuu wa Libya lililaaniwa pakubwa na jamii ya kimataifa. Hadi sasa watu zaidi ya 1090 wameuliwa  na wengine wasiopungua 5700 kujeruhiwa huko Tripoli tangu kuanza mashambulizi hayo tajwa. Libya ina mabunge mawili; moja likiwa na makao yake katika mji wa Tobrok mashariki mwa nchi na jingine huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo tangu miaka minne iliyopita kutokana na kuwepo hitilafu kati ya vyama na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo.