Genge la Daesh (ISIS) lafanya jinai mpya nchini Nigeria
Wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) wamesambaza mkanda wa video unaoonyesha mauaji ya watu 11 ndani ya Krismasi.
Katika mkanda huo wa video kundi hilo maarufu kwa kufanya jinai dhidi ya binaadamu, limedai kuwakata vichwa Wakristo 11 wa Nigeria. Hata hivyo taarifa za watu hao waliouawa hazijawekwa wazi, lakini inaelezwa kwamba watu hao walitekwa nyara wiki chache zilizopita katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Katika miaka ya hivi karibuni kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limepanua hatua zake za kigaidi huko magharibi mwa Afrika na hivi sasa limekita mizizi katika eneo la mpakani karibu na Ziwa Chad na nchi ya Niger.
Hii ni katika hali ambayo kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo lilianzisha hujuma zake mwaka 2009 nchini Nigeria, lilitangaza kuungana na genge la Daesh ambapo pia limeendelea kufuata nyayo zake katika kutenda jinai mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo.