Ujerumani: Wasioheshimu usimamishaji vita Libya wasusiwe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini amesema katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zinazopakana na Libya huko Algiers, mji mkuu wa Algeria kwamba, wale wote wasioheshimu usitishaji vita nchini Libya inabidi wawekewe vikwazo za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Televisheni ya Sky News imetangaza habari hiyo na kumnukuu Heiko Maas akisema hayo jana Alkhamisi tarehe 23 Januari 2020 akiongeza kuwa Berlin inaunga mkono juhudi zote zinazolenga kuutatua kisiasa mgogoro wa Libya.
Kikao hicho cha Algeria kimehudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumaini, Mali, Misri, Sudan, Chad, Nigeria na Tunisia na kimepewa jina la kikao cha majirani wa Libya.
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria aliitisha kikao hicho cha kutafuta suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Libya baada ya kufeli vikao viwili vya Moscow, Russia na Berlin, Ujerumani.
Siku ya Jumapili, viongozi walioshiriki kikao cha Berlin cha kutafuta amani ya Libya walikubaliana kuunda kamati maalumu ya kimataifa ya kusimamia usitishaji vita wa kudumu na utekelezaji wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya vilivyowekwa takriban miaka kumi iliyopita.
Hata hivyo muda mchache tu tangu kumalizika kikao cha Berlin, wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Misri na baadhi ya nchi za Magharibi walishambulia mji mkuu wa Libya, Tripoli ili kuonesha hawakujali yaliyoamuliwa kwenye kikao cha Berlin.
Mgogoro wa Libya ulizidi kuwa mkubwa baada ya janerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli mwezi Aprili 2019.