UN: Wasudan Kusini wanaunda idadi kubwa ya wakimbizi Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58755-un_wasudan_kusini_wanaunda_idadi_kubwa_ya_wakimbizi_ethiopia
Umoja wa Mataifa umesema raia wa Sudan Kusini ndio wanaounda idadi kubwa ya wakimbizi nchini Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2020 09:28 UTC
  • UN: Wasudan Kusini wanaunda idadi kubwa ya wakimbizi Ethiopia

Umoja wa Mataifa umesema raia wa Sudan Kusini ndio wanaounda idadi kubwa ya wakimbizi nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kufikia mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2019, Ethiopia ilikuwa mwenyeji wa wakimbizi wapatao 329,123 wa Sudan Kusini.

Kisut Gebregziabher, msemaji wa UNHCR nchini Ethiopia amesema nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambayo ni moja ya mataifa yenye idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika, ina wakimbizi zaidi ya 735,000 hivi sasa. Amesema mwaka jana pekee, jimbo la Gambella la Ethiopia liliwapokea wakimbizi wapya 8,219 kutoka Sudan Kusini.

Msemaji wa UNHCR nchini Ethiopia amesema Somalia ndiyo inayofuata kwa raia wake kuwa wakimbizi wengi nchini Ethiopia, ambapo kufikia mwishoni mwa mwaka 2019, nchi hiyo ilikuwa na wakimbizi 191,575 wa Kisomali.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Nchi nyingine ambazo raia wao wanaunda idadi kubwa ya wakimbizi nchini Ethiopia ni Eritrea wakimbizi139,281 na Sudan 42,285.

Msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa iisaidie Ethiopia kubeba mzigo wa kushughulikia maslahi ya wakimbizi hao, akieleza banaya kuwa wanahitaji dola milioni 658 kwa ajili ya kuwasidia wakimbizi hao mwaka huu 2020.