Magaidi kadhaa wauawa magharibi mwa Tunisia
Magaidi kadhaa wameuawa katika mapigano na vikosi vya usalama vya Tunisia magharibi mwa nchi hiyo.
Jeshi la Tunisia limetangaza Jumanne kuwa mapigano hayo yalijiri katika eneo la miinuko ya Kasserine ambapo wanajeshi wamekabiliana na kundi la magaidi. Taarifa hiyo imesema magaidi kadhaa wameuawa ingawa idadi ya waliouawa haikutajwa.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Jeshi la Tunusia lilituma askari katika eneo la Kasserine baada ya kupokea habari za kufika magaidi katika eneo hilo. Jeshi hilo limesema limetekeleza oparesheni kadhaa na kuwakamata magaidi katika maficho yao.
Tarehe 24 Novemba 2015, Tunisia ilitangaza hali ya hatari baada ya kutokea mripuko wa bomu katika basi lililokuwa na askari wa gadi ya rais, mjini Tunis.

Watu karibu 60 waliuawa wakiwemo watalii 59 kwenye mashambulizi mawili mengine yaliyofanywa na genge la kigaidi la ISIS katika miezi ya Machi na Juni 2015, nchini Tunisia.
Ikumbukwe kuwa raia wengi wa Tunisia wamejiunga na genge la kigaidi la ISIS na kufanya jinai na mauaji ya kutisha hasa katika nchi za Libya, Iraq na Syria.