HRW: Serikali imehusika na mauaji ya raia Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59411-hrw_serikali_imehusika_na_mauaji_ya_raia_cameroon
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeituhumu serikali ya Cameroon kuwa ilihusika na mauaji ya makumi ya raia katika jimbo linalozungumza Kiingereza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2020 22:56 UTC
  • HRW: Serikali imehusika na mauaji ya raia Cameroon

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeituhumu serikali ya Cameroon kuwa ilihusika na mauaji ya makumi ya raia katika jimbo linalozungumza Kiingereza.

Mtafiti wa masuala ya Afrika wa shirika hilo, Ilaria Allegrozzi amesema maafisa usalama wakishirikiana na wafugaji wa kabila la Fulani walihusika na mauaji hayo ya Februari 14 katika jimbo linalozungumza Kiingereza katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ambapo watu wasiopungua 22 waliuawa kikatili wakiwemo watoto wadogo 13 na wanawake wawili wajawazito.

Amesema, "mauaji hayo yalikuwa ya kinyama, mateso ya kutisha na ushahidi upo wazi. Mauaji hayo yalifanyika kwa makusudi na kwa mpangilio maalumu, kwa lengo la kuiadhibu jamii nzima kwa tuhuma za kuwahifadhi waasi wanaotaka kujitenga maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo."

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuitaka serikali ya Cameroon ifanye uchunguzi kuhusiana na mauaji  hayo katika kijiji cha Ngarbuh katika jimbo linalozungumza Kiingereza kaskazini mwa nchi.

Maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini Cameroon (Anglophone)

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 3,000 wameuawa nchini Cameroon tokea mwaka 2017 na wengine 530,000 kukimbia makazi yao kufuatia kuanza uasi katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. Wazungumzaji hao wa Kiingereza wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo wanaona ni vyema wapiganie kujitenga.