Serikali mpya ya Tunisia yapata ridhaa ya Bunge
Bunge la Tunisia limeipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali mpya ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh na hivyo kuhitimisha mkwamo wa uundaji serikali nchini humo.
Wabunge wa Tunisia jana usiku waliidhinisha serikali ya Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh kwa wingi wa kura ambapo Wabunge 129 waliipigia kura ya ndiyo serikali hiyo dhidi ya kura 77 za hapana.
Kupasishwa serikali hiyo kunahitimisha mzozo na mkwamo wa uundaji serikali uliokuwa ukiikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika hasa baada ya hatua zilizochukuliwa na Elyes Fakhfakh kutokiridhisha Chama cha al-Nahdha ambacho ndicho chenye viti vingi katika Bunge la Tunisia.
Elyes Fakhfakh aliteuliwa na kupewa jukumu la kuunda serikali, baada ya Habib al-Jemli aliyekuwa Waziri Mkuu mteule kushindwa kupata kura za kuwa na imani naye katika Bunge la nchi hiyo.
Matukio haya yanatokea miezi kadhaa baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Tunisia ambapo Kais Saied aliibuka mshindi na kuwa Rais mpya wa nchi hiyo. Katika kinyang'anyiro cha Bunge, Chama cha al-Nahdha kilizoa viti vingi vya Bunge na hivyo kuifanya anga ya siasa nchini Tunisia kuwa tata.
Wiki iliyopita Rais wa Tunisia alitishia kuwa, atalivunja Bunge la nchi hiyo na kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati kwa mujibu wa kipengee cha 89 cha katiba ya nchi hiyo endapo serikali ya Elyes Fakhfakh itashindwa kupata kura za kuwa na imani nayo.