Jeshi la Cameroon lasema limeua 'magaidi' wanaotaka kujitenga
Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa, 'magaidi' wa harakati ya kutaka kujitenga katika eneo linalozungumza Kiingereza wameuawa katika operesheni ya jeshi la nchi hiyo.
Waziri wa Habari, Rene Emmanuel Sadi amesema waasi hao wa kundi la Ambazonia wanaotaka kujitenga maeneo yanayozungumza Kiingereza magharibi mwa nchi wameuawa katika operesheni ya mwisho wa wiki na wanajeshi wa nchi hiyo, huku akikanusha ripoti za baadhi ya vyombo vya habari kwamba waliouawa ni raia.
Amesema, "magaidi kumi wanaotaka kujitenga wakiwemo wanawake watatu waliuawa katika eneo la Small Babanki, kaskazini magharibi mwa nchi. Habari za kuuawa raia wakiwemo wanawake na watoto wadogo kwenye operesheni hiyo hazina msingi wowote na ni propaganda."
Haya yanajiri siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kuituhumu serikali ya Cameroon kuwa ilihusika na mauaji ya makumi ya raia katika jimbo linalozungumza Kiingereza.
Mtafiti wa masuala ya Afrika wa shirika hilo, Ilaria Allegrozzi alisema maafisa usalama wakishirikiana na wafugaji wa kabila la Fulani walihusika na mauaji hayo ya Februari 14 katika jimbo linalozungumza Kiingereza katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ambapo watu wasiopungua 22 waliuawa kikatili wakiwemo watoto wadogo 13 na wanawake wawili wajawazito.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 3,000 wameuawa nchini Cameroon tokea mwaka 2017 na wengine 530,000 kukimbia makazi yao kufuatia kuanza uasi katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza, ambao wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu huku wakinyimwa haki zao kama raia wa Cameroon, hivyo wanaona ni vyema wapiganie kujitenga.