Ethiopia: Hatutaburuzwa na Marekani kusaini makubaliano ya bwawa la Nahdha
Ethiopia imesema haitakubali kushinikizwa na Marekani kutia saini makubaliano ya mpango wa Washington kuhusu bwawa la al-Nahdha.
Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Gedu Andargachew, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia amesema, nchi tatu zinazohusika na mgogoro juu ya bwawa hilo zinaweza kuupatia ufumbuzizi mzozo uliopo pasina mashinikizo ya nje.
Amesema, "Marekani ni nchi mtazamaji katika mgogoro huu, tunaamini kuwa, makubaliano yanayofikiwa chini ya mashinikizo hayana maslahi kwa upande wowote wa mazungumzo hayo."
Tarehe 29 Februari, kulifanyika mkutano mjini Washington ambao ulisusiwa na Ethiopia na ndani ya mkutano huo kulitiwa saini makubaliano ya mpango wa Marekani kuhusu bwawa la al-Nahdha.
Ethiopia ilitangaza kupinga mpango huo, ikaishambulia taarifa iliyotolewa na Marekani ya kutaka kuanza tena mazungumzo kuhusu ujenzi wa bwawa la al-Nahdha unaotajwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa umeme barani Afrika.
Ethiopia ilianza kujenga bwawa la al-Nahdha mwaka 2011 suala ambalo liliikasirisha Misri ikidai kuwa mradi huo utapunguza sana maji yanayoingia Misri kutoka Mto Nile. Hivi karibuni, Sudan ilizitaka Misri na Ethiopia kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutatua mgogoro wa bwawa la al Nahdha la nchini Ethiopia.