Watu 15 wauawa katika mlipuko wa bomba la gesi Lagos Nigeria
(last modified Mon, 16 Mar 2020 08:07:31 GMT )
Mar 16, 2020 08:07 UTC
  • Watu 15 wauawa katika mlipuko wa bomba la gesi Lagos Nigeria

Mlipuko wa bomba la gesi uliotokea katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos nchini Nigeria umepelekea kwa uchache watu 15 kuaga dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Mlipuko huo uliotokea jana umeharibu na kubomoa takribani majengo 50 huku magari, malori na pikipiki zikiharibiwa pia katika mlipuko huo. Aidha hoteli na shule moja zilizoko karibu na eneo ulipotokea mlipuko huo nazo zimeharibiwa vibaya

Ibrahim Farinloye, msemaji wa Kitengo cha Taifa cha Huduma za Dharura ameziambia duru za habari kwamba, miili 15 imepatikana katika eneo la tukio huku majengo 50 ya karibu na eneo hilo yakibomolewa katika Wilaya ya Abule Ado mjini Lagos.

Baadhi ya wahanga wa mlipuko huo walikuwa njiani kuelekea kanisani ambapo miongoni mwa waliofariki dunia katika tukio hilo ni watu wanne wa familia moja.

Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria limetangaza kuwa, mlipuko huo ulisababishwa na gari moja lililokwenda na kugonga bomba la kusafirishia gesi.

Mlipuko mkubwa uliotokea na kuharibu nyumba za karibu na eneo hilo umesababisha maafa na uharibifu mkubwa, imeeleza taarifa ya Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria.

Milipuko ya mabomba ya mafuta na gesi nchini Nigeria imekuwa ikitokea mara kwa mara katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na kusababisha maafa na uharibifu wa mali.