Vyama vya Waislamu nchini India vyalalamikia kutiwa mbaroni vijana wa Kiislamu
Chama cha Jumuiya ya Maulama nchini India kimetangaza kuwa, uchunguzi unaonyesha kuwa katika siku za hivi karibuni vijana wa Kiislamu wametiwa mbaroni kwa namna iliyoratibiwa na kupelekwa maeneo yasiyojulikana.
Ripoti kutoka India zinaarifu kwamba, katika kikao na mkuu wa jeshi la polisi mjini New Delhi wawakilishi wa Jumuiya ya Maulama nchini humo wameonyesha wasi wasi wao mkubwa juu ya wimbi la kutiwa mbaroni Waislamu. Viongozi wa jumuiya hiyo wamebainisha kwamba uchunguzi wao unaonyesha kuwa, utiwaji mbaroni vijana hao wa Kiislamu unatekelezwa kwa namna iliyoratibiwa. Wamesisitiza kuwa, kutiwa mbaroni vijana Waislamu na bila kuzingatia wahusika wakuu wa mauaji ya kutisha ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na vijana wa Kihindu, ni jambo la kutia wasi wasi mkubwa kuhusiana na mtazamo wa kibaguzi wa serikali dhidi ya raia Waislamu wa nchi hiyo. Licha ya polisi ya India kutoa ahadi ya kufuatilia suala hilo, lakini vyama vya Waislamu vinaamini kwamba maadamu hakujaangaliwa upya sheria ya uraia, matatizo hayo yataendelea kushuhudiwa.
Hivi karibuni na sambamba na safari ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini India, askari wa nchi hiyo kwa kushirikiana na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada, waliwashambulia Waislamu ambapo kwa akali waliwaua 50 kati yao na kuwajeruhi wengine 400. Licha ya kupita wiki mbili tangu kujiri tukio hilo, serikali bado haijachukua hatua yoyote muhimu ya kuwatia mbaroni wahusika wa jinai hiyo.