Tripoli yaitaka Khartoum kuwaondoa mamluki wa Kisudani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59881-tripoli_yaitaka_khartoum_kuwaondoa_mamluki_wa_kisudani_nchini_libya
Mjumbe katika Baraza la Utawala la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, Muhammad Ammari amesema Libya ingali inasubiri ufafanuzi wa Serikali ya Sudan kuhusu uwepo wa mamluki wa Kisudani katika safu za wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftar wanaoendelea kuhujumu mji wa Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2020 07:17 UTC
  • Tripoli yaitaka Khartoum kuwaondoa mamluki wa Kisudani nchini Libya

Mjumbe katika Baraza la Utawala la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, Muhammad Ammari amesema Libya ingali inasubiri ufafanuzi wa Serikali ya Sudan kuhusu uwepo wa mamluki wa Kisudani katika safu za wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftar wanaoendelea kuhujumu mji wa Tripoli.

Ammari ameitaka serikali ya Sudan kuwarejesha nyumbani mara moja mamluki hao wa Kisudani na kutishia kwamba, iwapo wanamgambo hao wataendelea kushiriki katika hujuma inayolenga mji mkuu wa Libya, watarejeshwa Sudan wakiwe kwenye majeneza.

Muhammad Ammari amesema kuwa idadi ya mamluki wa Kisudan waliouawa nchini Libya ni kubwa hususan baada ya mapigano makali yaliyotokea eneo la Ain Zara kusini mwa mji wa Tripoli, Ijumaa ya jana.

Mapigano ya ndani Libya

Afisa huyo wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya amesema uchunguzi uliofanywa na mateka wa Kisudani waliokamatwa Libya kutoka kwenye mamluki wa kundi la Janjaweed unathibitisha kuwapo kwa mamluki wa Kisudani katika wapiganaji wa jenerali mstaafu Khalifa Haftar na kwamba Imarati ndiyo inayowaajiri na kuwatuma mamluki hao kupiganaji nchini Libya.

Alkhamisi ya juzi peke yake jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya lilitangaza kuwa limewaangamiza mamluki 24 wa kundi la Janjaweed kutoka Sudan wanaopigana katika safu za Haftar na wengine kadhaa wameshikwa mateka.