Wapiganaji wa Haftar wapuuza mwito wa UN, waendelea kumwaga damu Libya
Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imetangaza habari ya kuuawa watu 6 katika mashambulizi ya roketi ya kundi la wanamgambo linalojiita jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar jana Jumatatu viungani mwa mjini mkuu Tripoli.
Amin al-Hashemi, msemaji wa Wizara ya Afya ya serikali hiyo inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa amesema raia sita wakiwemo watu wawili wa familia moja wameuawa katika hujuma hizo za jana, baada ya vikosi vya Haftar kushambulia kwa maroketi makazi ya watu kusini mwa Tripoli.
Ameongeza kuwa, wafanyakazi wawili ambao ni wahajiri wameuawa katika shambulizi jingine la roketi karibu na Uwanja wa Ndege wa Mitiga mjini Tripoli, mbali na mwanamke mwingine kuuawa baada ya roketi kuangukia paa la nyumba yake katika kijiji cha Tajoura, viungani mwa Tripoli.
Hata hivyo wapiganaji hao wa Haftar wanadai kuwa, walitekeleza hujuma hizo baada ya wanajeshi wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kushambulia mji wa Tarhuna karibu na Tripoli kwa maroketi aina ya Grad.
Mashambulizi hayo yamejiri masaa machache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kukaribisha jibu chanya la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya na la wanamgambo wanaoongozwa na Haftar kwa ajili ya kusimamisha mapigano nchini humo, kutokana mripuko wa ugonjwa wa corona.
Wiki iliyopita pia, mabinti watano wenye umri wa miaka 14 hadi 20 waliuawa huku wasichana watano akiwemo wa miaka 11 wakijeruhiwa vibaya baada ya wanamgambo wa Haftar kushambulia kwa mabomu maeneo ya Ain Zara na Bin Ghahsir kusini mwa Tripoli. Hali ya mchafukoge huko Libya imepelekea kushindwa kutangazwa hadi sasa takwimu kuhusu hali ya maambukizo ya corona nchini humo.
Tokea Aprili mwaka jana wakati Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, maelfu ya watu wakiwemo watoto wadogo na wanawake wameuawa na kujeruhiwa, mbali na wengine 150,000 kuachwa bila makao.