Vikosi vya Haftar vyadai vimetungua drone 2 za Uturuki huko Libya
Kundi la wanamgambo wanaojiita Jeshi la Tifa la Libya wanaoongozwa na jenerali Khalifa Haftar linadai kuwa limetungua ndege mbili zisizo na rubani za Uturuki zilizokuwa zikiruka katika anga ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Hayo yalisemwa jana na Ahmed Mismari, msemaji wa 'Jeshi la Tifa la Libya' ambaye alidai kuwa, drone ya kwanza ya Uturuki ilitunguliwa ikiruka karibu na kambi ya jeshi ya Okba Ibn Nafa magharibi mwa Libya mpakani na Tunisia.
Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mismari amesema ndege ya pili isiyo na rubani ya Uturuki imetunguliwa ikiruka katika makao makuu ya wilaya ya Ain Zara, kusini mashariki mwa mji mkuu, Tripoli.
Vikosi vya Haftar vimepuuza miito ya jamii ya kimataifa ya kusitisha vita na mashambulizi yake wakati huu wa kukabiliana na virusi vya Corona.
Hii ni katika hali ambayo, hapo jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alilaani vikali shambulio lililofanywa na wanamgambo hao watiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya hospitali ya kulazwa wagonjwa wa virusi vya Corona kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kusisitiza kuwa, mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa sekta ya afya ni jinai za kivita.
Tangu mwezi Aprili 2019, kundi la Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar ambalo linaungwa mkono na Imarati, Saudi Arabia, Russia, Misri na Jordan lilianzisha hujuma na mashambulio dhidi ya Tripoli; na kuanzia Desemba 12 mwaka huo likashadidisha mashambulio yake kwa lengo la kuuteka mji mkuu huo wa Libya unaodhibitiwa na vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayotambulika rasmi kimataifa.