Wagonjwa wapya 14 wa COVID-19 wabainika nchini Tanzania
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kuwa, watu 14 ambao wote ni raia wa Tanzania wamepatikana na ugonjwa wa corona na kufanya idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 nchini humo kufikia 46.
Waziri Ummy ametoa ufafanuzi zaidi kwa kusema, kati ya wagonjwa hao 14, 13 wanatoka jijini Dar es Salaam na mmoja yuko Arusha. Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto wa Tanzania vile vile amesema, wagonjwa hao wanaendelea kupatiwa matibabu na wamewekwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya.
Aidha wataalamu wa afya wanaendelea kuwatafuta watu walioshirikiana na wagonjwa hao ili kuwapima kuona kama wamepata maambukizo ya virusi hivyo. Wakati huo huo Waziri Ummy ameendelea kuwataka wananchi kuchukua tahadhari zote za kiafya ili kujikinga na maambukizo ya virusi hivyo vya Corona.