Wanamgambo 1,500 wa Kisyria wawasili Libya kushirikiana na Haftar
Vikosi vya jeshi la Khalifa Haftar vimetangaza kuwa wanamgambo 1,500 wa Kisyria wamewasili Tripoli wakisaidiwa na Uturuki.
Ahmed al-Mismari ambaye ni msemaji wa kundi la Haftar la Libyan National Army amesema kuwa wanamgambo 1,500 kutoka Syria wamewasili kwa meli kwenye bandari ya Tripoli wakitokea Uturuki.
Ahmed al-Mismari ameongeza kuwa, wapiganaji hao wamewasili Libya wakiwa na silaha licha ya kwamba azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga marufuku uingizaji wa silaha nchini humo.
Msemaji wa jeshi la Khalifa Haftari amesema kuwa, viwanja vya ndege vya Uturuki pia vimekuwa vikitumiwa kila siku kupeleka mamluki katika maeneo ya Misrata na Tripoli. Ameongeza kuwa ndege zisizo na rubani za Uturuki pia zinalenga na kushambulia misafara ya shehena za misaada ya kibinadamu na dawa nchini Libya.
Wakati huo huo shirika la habari la Anadolu limeripoti kuwa, vikosi vya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya Jumapili ya jana vilizima shambulio la jeshi la Haftar katika eneo la Abu Farin huko mashariki mwa mji wa Tripoli na kuua wapiganaji wasiopungua 35.
Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Aprili 2019, vikosi vya Haftar vinavyosaidiwa na Saudi Arabia, Imarati na Misri pamoja na baadhi ya nchi za Magharibi vilianzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuuteka mji huo unaodhibitiwa na vikosi vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.
Zaidi ya watu 1,500 na wengine wasiopungua 6.000 wamejeruhiwa tangu vikosi vya Khalifa Haftari vilipoanzisha mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli.