Ripoti: UAE inashirikiana na Sudan kuunga mkono waasi wa Haftar nchini Libya
Gazeti moja la Libya limefichua kuhusu mapatano mapya ya Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa lengo la kumuunga mkono kinara wa waasi Libya, Jenerali Khalifa Haftar.
Gazeti la Libya Observer limenukulu duru za kuaminika zikifichua kuwa, Kamandi ya Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Sudan imeafiki ombi la UAE la kutuma askari katika mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kumuokoa Khalifa Haftar.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, UAE imeahidi kuunga mkono kijeshi na kifedha Kamandi ya Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Sudan kutokana na ushirikiano huo.
Hivi sasa maelfu ya wanajeshi wa Sudan wako vitani Libya wakiwasaidia wanamgambo wa Haftar ambao wanajiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' lakini serikali ya Sudan inakanusha kuwepo askari wake nchini Libya.
Hivi karibuni Televisheni ya Al Jazeera ilisema kuna ushahidi wa kutosha kuwa Jeshi la Angal la Sudan lintumika kuwahamisha mamia ya wapiganaji wa Libya.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni walisema wapiganaji kutoka Darfur Sudan hivi sasa wanatumika kama mamluki wa Haftar nchini Libya.
Tarehe 4 Aprili 2019, kundi la Khalifa Haftar lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya mji mkuu wa Libya Tripoli kwa tamaa ya kuuteka mji huo na kuipindua Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa. Hata hivyo ndoto hiyo haijatimia hadi leo hii.
Baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani na hivi sasa kuna serikali mbili hasimu, moja ya mashariki na nyingine ya magharibi mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya pande hizo mbili vinaendelea kupigana.
Serikali hizo mbili hasimu ziliibuka mwaka 2014 ambapo moja ina makao makuu yake mjini Tobruk, mashariki mwa nchi na inaungwa mkono na Jenerali muasi Khalifa Haftar, na nyingine ni Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na ambayo inasimamia maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo ukiwemo mji mkuu, Tripoli.