May 01, 2020 13:40 UTC
  • Wafuasi 23 wa Omar al Bashir watiwa mbaroni nchini Sudan

Polisi nchini Sudan wamewatia mbaroni wafuasi 23 wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Mtandao wa habari wa Eremnews wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wafuasi hao wa Omar al Bashir wamekamatwa katika maandamano ya kumuunga mkono rais huyo wa zamani wa Sudan. Waandamanaji hao wameandamana mjini Khartoum ili kushinikiza kuachiliwa huru al Bashir kutoka kizuizini.

Makumi ya viongozi wa zamani wa Sudan wako kiziuzini hivi sasa  kwa tuhuma za kutenda jinai na makosa mengine ya kisiasa.

Tangu mwezi Disemba 2018, Sudan ilikumbwa na maandamano makubwa ya wananchi waliolalamikia utendaji mbovu wa serikali ya Omar al Bashir. Maandamano hayo yaliendelea hadi mwezi Aprili 2019 wakati jeshi lilipoingilia kati likamuondoa kwa nguvu madarakani Omar al Bashir. Baada ya hapo ilifuatia miezi kadhaa ya maandamano ya wananchi hadi jeshi lilipolazimika kuunda serikali ya mpito na kuvunja Baraza la Kijeshi lililoundwa baada ya kupinduliwa al Bashir. Tangu wakati huo hadi hivi sasa Omar al Bashir na viongozi kadhaa wa serikali yake wako kizuizini.

Maandamano mjini Khartoum Sudan

 

Habari nyingine kutoka Sudan inasema kuwa, jeshi la nchi hiyo limekanusha habari ya kanali ya televisheni ya al Jazeera ya Qatar iliyosema kuwa, wanajeshi wa Sudan wametumwa nchini Libya. 

Msemaji wa jeshi la Sudan, Brigedia Jenerali Amir Mohamed al Hassan amesema kuwa, kanali ya televisheni ya al Jazeera inapotosha watazamaji wake kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu Sudan. Vile vile ametishia kuichukulia hatua za kisheria televisheni ya al Jazeera ya Qatar.

Tags