Tunisia yarefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi sita zaidi
Ofisi ya Rais wa Tunisia imetoa tangazo maalumu la kurefusha hali ya hatari ya nchi nzima kwa muda wa miezi sita mingine.
Kwa mujibu wa televisheni ya "Rusia al Yaum," Ofisi ya Rais wa Tunisia imesema, Rais Kais Saied wa nchi hiyo amerefusha muda wa hali ya hatari kuanzia leo Jumamosi tarehe 30 Mei hadi tarehe 25 Novemba mwaka huu.wa 2020.
Kabla ya hapo pia, yaani mwezi Aprili mwaka huu, Tunisia ilirefusha kwa muda wa mwezi mmoja hali hiyo ya hatari ya nchi nzima.
Hali ya hatari ya nchi nzima huko Tunisia ilitangazwa tarehe 24 Novemba 2015 baada ya magaidi kufanya mashambulizi yaliyoua na kujeruhi watu 30. Tangu wakati huo hadi leo hii muda huo umekuwa ukirefushwa kila unapokaribia kumalizika.
Katika shambulio hilo la mwaka 2015, magaidi wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) walishambulia basi la askari wa gadi ya Rais katika mji mkuu Tunis na kuua maafisa 12 wa gadi hiyo.
Hali ya hatari nchini Tunisia inawapa haki viongozi kuchukua hatua za dharura kama vile kuendesha operesheni za kuwaweka watu kizuizini, kupiga marufuku mikutano, kutangaza amri ya kutotoka nje, kudhibiti vyombo vya habari, kuzuia mikusanyiko na kuchuja habari kwa idhini ya mahakama.
Hatua hiyo imekuja katika hali ambayo mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Rais Kais Saied wa nchi hiyo alitoa amri ya kuachiwa huru wafungwa 1,420 baada ya kuenea maambukizi ya kirusi cha corona ikiwa kama tahadhari ya kupunguza maambukizi ya COVID-19 katika jela za nchi hiyo.