Wapiganaji wa Haftar: Uturuki imetuma vifaru nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61381-wapiganaji_wa_haftar_uturuki_imetuma_vifaru_nchini_libya
Wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar nchini Libya wamesema kwamba meli moja ya mizigo kutoka Uturuki imeshusha vifaru visivyojulikana idadi yake aina ya M60 kwa ajili ya serikali ya wokovu wa kitaifa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 03, 2020 04:35 UTC
  • Wapiganaji wa Haftar: Uturuki imetuma vifaru nchini Libya

Wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar nchini Libya wamesema kwamba meli moja ya mizigo kutoka Uturuki imeshusha vifaru visivyojulikana idadi yake aina ya M60 kwa ajili ya serikali ya wokovu wa kitaifa ya nchi hiyo.

Mtandao wa habari wa Libya Al-Youm umemnukuu Ahmed Al-Mismari, Msemaji wa wanamgambo wa Haftar wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya na wenye makao yao kaskazini mwa nchi hiyo akisema kwamba, wapiganaji wake walifuatilia meli ya mizigo ya Uturuki ikipakua vifaru aina ya M60 kwenye bandari ya Misrata. Kwa mujibu wa wapiganaji wa Haftar meli hiyo iliyotia nanga katika bandari ya Misrata, inamilikiwa na moja ya mashirika ya Uturuki na kwamba ilifuatiliwa hadi kwenye bandari hiyo.

Khalifa Haftar anayeungwa mkono na nchi za Saudia, Imarati, Misri nk

Tangu bunge la Uturuki lipitishe muswada wa kutumwa askari wa nchi hiyo Libya, imekuwa ikiiunga mkono kisiasa na kijeshi serikali ya mwafaka wa kitaifa ambayo inatambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa. Ripoti zinaarifu kwamba kabla ya hapo pia serikali ya Ankara ilituma nchini Libya kwenda kwa serikali ya Fayez al-Sarraj, magari na droni za kijeshi pamoja na zana nyingine kama vile makombora ya ardhi kwa anga. Wapiganaji wa Haftar wanaungwa mkono na nchi kama vile Saudi Arabia, Misri, Imarati na Ugiriki.