Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yadhibiti kikamilifu mji wa Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61409-serikali_ya_mwafaka_wa_kitaifa_libya_yadhibiti_kikamilifu_mji_wa_tripoli
Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya imetangaza kwamba imefanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli na kufurusha mabaki ya wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftari.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2020 07:41 UTC
  • Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yadhibiti kikamilifu mji wa Tripoli

Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya imetangaza kwamba imefanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli na kufurusha mabaki ya wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftari.

Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imesema kuwa, sasa maeneo yote ya mji wa Tripoli yanadhibitiwa na jeshi la taifa na yamekombolewa kuoka mikononi mwa wapiganaji wa Haftar.

Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, Muhammad Qanunu amethibitisha kwamba, wapiganaji wa serikali wanaudhibiti kikamilifu mji wa Tripoli.

Ripoti zinasema wapigajani wa jenerali Haftar jana Jumatano walilazimika kurudi nyuma na kuondoka katika maeneo ya Wadi Rabie na Ain Zara baada ya kupoteza udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Tripoli. 

Ushindi huo wa jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kifaifa nchini Libya una maana ya kufurushwa kikamilifu wapiganaji wa Khalifa Haftar kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo. 

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya imedhibiti mji wa Tripoli.

Askari wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar tokea mwezi Aprili 2019 wamekuwa wakiushambulia kwa makombora na mizingi mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuudhibiti na kuutoa mikononi mwa serikali halali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj.

Hata hivyo mapambano makali ambayo yamekuwa ya askari wa serikali hiyo yamefelisha njama na hujuma zote ambazo zimekuwa zikifanywa kwa msaada wa nchi za Magharibi na za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia, Imarati na Misri.

Nchi hizo tatu za Kiarabu zikisaidiwa kwa karibu na Ufaransa zinawasaidia kijeshi askari wa Haftar, huku Uturuki, Italia, Qatar na Umoja wa Mataifa zikiiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyo na makao makuu mjini Tripoli.