Idadi ya walioaga dunia katika ajali ya boti Tunisia yaongezeka
Idadi ya wahajiri waliopoteza maisha katika ajali ya boti iliyotokea hivi karibuni katika mji wa pwani wa Sfax nchini Tunisia imeongezeka na kufikia watu 54.
Jeshi la Majini la Tunisia na wapigambizi wanasema hadi hivi sasa miili 54 ya wahajirii hao imeshaopolewa kutoka baharini. Boti hiyo ilitazamiwa kutia nanga leo Jumamosi katika pwani ya Ugiriki kabla ya kuzama siku ya Alkhamisi.
Ali Ayadi, Mkurugenzi wa Afya katika eneo la Sfax amethibitisha habari za kutokea ajali hiyo na kusema kuwa, hadi hivi sasa miili 54 ya watu waliozama kwenye ajali hiyo imeshaopolewa kutoka majini na kwamba watu kadhaa waliobakia hawajapatikana hadi hivi sasa.
Naye msemaji wa mahakama ya eneo la Sfax, Murad al-Turki amesema akthari ya wahajiri waliofariki dunia katika ajali hiyo ni raia wa nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika.
Julai mwaka jana, mtumbwi mmoja uliokuwa umejaza wahajirii kupita kiasi ulizama karibu na fukwe za Tunisia ambapo watu zaidi ya 80 walipoteza maisha.
Wahajiri wengi haswa kutoka nchi za Afrika hupotea na kuzama baharini kila mwaka katika fukwe za Tunisia wakijaribu kuvuka kimagendo kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kupata maisha mazuri, huku baadhi yao wakikimbia machafuko ya kisiasa na kijamii katika nchi zao.
Sababu nyingine ya kushuhudiwa wimbi hilo la wahajiri haramu ni uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.