Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi ufanyike kuhusu makaburi ya umati Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kushtushwa kwake kutokana na kugundulika kwa makaburi ya umati nchini Libya katika siku za hivi karibuni, katika eneo ambalo hivi karibuni lilikuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo wanaojiita Libyan National Army (LNA) ambao wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulitangaza Alhamis ya tarehe 11 mwezi huu wa Juni kuwa kumegundulika takribani makaburi matano huko Tarhouma, kilomita kama 100 hivi kusini mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Mji huo ulikuwa ngome ya vikosi vya Jenerali Haftar wakati wa kampeni za kuiteka Tripoli, kampeni ambayo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake Tripoli hivi karibuni walifanikiwa kuchukua udhibiti wa mji huo baada ya kuwatimua wanamgambo wa Haftar wanaopata himaya ya Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudia na baadhi ya nchi za Magharibi.
Katika taarifa aliyoitoa kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu Guterres anasema anatoa wito “ufanyike uchunguzi wa kina na wa wazi”, na waliotekeleza mauaji hayo wafikishwe mbele ya sheria.
Guterres amezitaka mamlaka nchini Libya kuyalinda maeneo yaliyogundulika kuwa na makaburi ya umati, kuwatambua walioathirika, kutambua chanzo cha kifo na kuirejesha miili kwa ndugu zao. Wakati huo huo Serikali ya Muafaka imesema wapiganaji wa Haftar wametekeleza mauaji ya umati ya raia na imetoa wito kwa umoja wa mataifa kuchunguza jinai hiyo. Taarifa hiyo imesema mauaji hayo ya umati yalijiri katika miji ya Tarhouna na Qaser Bin Ghashir na kwamba waliouawa walizikwa katika makaburi ya umati.