HRW yataka uchunguzi kuhusu jinai za Jenerali Haftar nchini Libya
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetaka kufanyike uchunguzi wa kina kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar nchini Libya.
Shirika la habari la AFP limeripoti habari kutoka mjini Tripoli na kulinukuu shirika la Human Rights Watch likisema kuwa, kuna ushahidi wa wazi na wa kutosha unaothibitisha kuteswa na kuuliwa kiholela watu kulikofanywa na wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar na limetaka kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu jinai za kivita ambazo inaaminika zimefanywa na wanamgambo hao.
Shirika hilo pia limesema katika ripoti yake kwamba inabidi kufanyike uchunguzi wa kina kuhusiana na ushahidi wa wazi uliopo kuhusu mateso, kuuliwa kiholela, kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima miili ya maiti waliouliwa na wanamgambo wa Libya walioko chini na jenerali Haftar. Jinai hizo inaaminika zimefanywa na wanamgambo hao wa Haftar katika viunga vya Tripoli, mji mkuu wa Libya.
Shirika la Human Rights Watch pia limesema mikanda ya video iliyochukuliwa mwezi Mei mwaka huu wa 2020 na kuenea kwenye mitandao ya kijamii inaonesha kuwa wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar ndio waliofanya jinai hizo.
Ripoti ya shirika hilo imeongeza kuwa, mateso waliyofanyiwa watu waliotekwa na wanamgambo hao na kuuliwa kiholela ni ushahidi na dhihirisho la wazi wa jinai za kivita.
Kuanzia mwezi Aprili 2019 jenerali muasi Khalifa Haftar alianzisha mashambulizi makubwa ya kutaka kuuteka mji mkuu wa Libya Tripoli kwa nia ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa. Hata hivyo ndoto hiyo haikuaguka bali wanamgambo hao wamefurushwa kwenye maeneo yote waliyokuwa wameyateka baada ya kushindwa mfululizo na kwa wiki kadhaa.