Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yapinga kikao cha Arab League
Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya amesema kuwa, Tripoli inapinga kufanyika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kuhusu masuala ya nchi hiyo.
Toleo la mtandaoni la gazeti la al Arabi al Yaum limemnukuu Mohamed Taher Siala, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya akisema kuwa nchi yake haikubaliani na uamuzi wa kuitishwa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Arab League kuhusu Libya. Ikumbukwe kuwa Misri ndiyo iliyoitisha kikao hicho.
Akizungumza kwa njia ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Oman, Yusuf bin Alawi, Bw. Siala amesema, Libya imepinga mwaliko wa Misri wa kushiriki katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu uliopangwa kufanyika kwa njia ya Intaneti.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya pia ametoa sababu za kupinga kikao hicho akisema, ni kweli maudhui ya kikao ni Libya lakini Misri haikuheshimu protokali za kuitisha kikao hicho na hata haikushauriana na Tripoli kuhusu jambo hilo.
Hivi karibuni serikali ya Misri imetaka kufanyike kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuzungumzia matukio ya hivi karibuni ya Libya.
Ikumbukwe kuwa Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Magharibi hasa Ufaransa zinamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye katika kipindi cha wiki za hivi karibuni ameshindwa vibaya kwenye vita vya ndani ya Libya.
Mwezi Aprili mwaka jana 2019, Jenerali Khalifa Haftar alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa ndoto ya kuipindua Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa, lakini ndoto hiyo imeshindwa kuaguka, bali jenerali huyo na waungaji wake mkono wameshindwa vibaya na wamepoteza maeneo yote waliyokuwa wameyateka katika kampeni yao hiyo iliyoanzia mwezi Aprili, 2019.