Serikali ya Libya: kukombolewa Sirte na Jufra ni jambo la dharura
Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) imesema kuwa suala la kukomboa miji ya Sirte na Jufra kutoka mikononi mwa wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar ni jambo lenye udharura mkubwa baada ya kutumwa mamluki wa kigeni nchini humo.
Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa, Muhammad Qanunu amesema kuwa mji wa Sirte ni eneo hatari zaidi baada ya kuwa kitovu cha mamluki wa kampuni ya Wagner ya Russia. Qanunu amewataja mamluki hao kuwa ni "magenge ya uhalifu."
Juzi Jumamosi pia Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alizitaka Marekani na Umoja wa Ulaya kuziwekea vikwazo pande nyingine husika katika mgogoro wa Libya na mamluki wa kigeni.
Libya ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2011 baada ya majeshi ya nchi za Magharibi NATO kuivamia nchi hiyo kufuatia uasi wa wananchi uliopeleka kuuliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi. Katika kipindi cha miaka 9 iliyopita nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na serikali mbili tofauti, ile yenye makao yake mjini Tripoli inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa, na serikali ya Tobruk ikiongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar. Serikali hii ya Haftar inasaidiwa na nchi kama Saudi Arabia, Misri, Ufaransa na Imarati. Hali hii imeupa sura ya kimataifa mgogoro wa ndani wa Libya.