Lavrov: Haftar yuko tayari kusaini makubaliano ya kusitisha vita nchini Libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa wanamgambo wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya wako tayari kusaini makubaliano ya kusitisha vita nchini humo.
Sergei Lavrov amesisitiza kuwa kundi la wanamgambo hao wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar liko tayari kusaini makubaliano ya kusimamisha vita. Amesema Moscow inashirikiana na Uturuki juu ya namna ya kufikiwa makubaliano hayo nchini Libya.
Lavrov ameongeza kuwa Khalifa Haftar yuko tayari kusaini makubaliano ya kusitisha vita na kwamba Moscow inaratajia kwamba Uturuki itafanikiwa kuishawishi Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya pia kusiani makubaliano hayo.
Mapigano ya ndani nchini Libya yameongezeka katika siku za karibuni kati ya wanajeshi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar.
Itakumbukwa kuwa, Uturuki inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj. Misri, Imarati, Saudi Arabia, Ufaransa na Ugiriki zinamuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar. Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2015.