Wataalamu wa UN waitaka Tanzania isitishe ukandamizaji
Wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wameitaka Tanzania isitishe hatua zinazobinya uhuru wa umma, hususan wakati huu ambapo nchi hiyo ya Afrika Mashariki inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Katika taarifa siku ya Jumatano mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao watatu, David Kaye, Clément Nyaletsossi Voule na Mary Lawlor wameisihi serikali ya Tanzania izingatie ahadi zake kuhusu haki za kibinadamu za kimataifa.
Wataalamu hao wamebainisha wasiwasi kuhusu utekelezaji wa marekebisho ya sheria ambayo itadhibiti uwezo wa mashirika ya kiraia na watu binafsi kutetea haki za makundi yaliyo hatarini, na jamii na hivyo kukiuka uhuru wa kujumuika.
Wataalamu hao pia wamesema hatua hizo zinakuja huku viongozi wanane wa upinzani wakiwa wamekamatwa kwa kukusanyika kinyume cha sheria.
Wamesema vitisho na manyanyaso dhidi ya wanaharakati na wakosoaji wa serikali havikubaliki na hivyo visitishwe mara moja.
Hali kadhalkika wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema vyombo vya habari nchini Tanzania viko chini ya mashinikizo makubwa na kusema, 'kufuatia amri ya serikali, vyombo vya habari vinavyomkosoa Rais na Serikali vinatozwa faini au kusimamishwa.'
Hayo yanajiri huku Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akiwa amevitaka vyombo vya ulinzi nchini humo visitumie nguvu mahala ambapo hapastahili kutumia nguvu huku akiamini vyama vya siasa vitafanya kampeni za uchaguzi kistaarabu.
Akizungumza Jumatano wakati wa uzinduzi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jijini Dodoma Rais Magufuli aidha amevitaka vyama vya siasa kutovichokoza vyombo vya usalama na ulinzi na kutofanya mambo ambayo yatavifanya vitumie nguvu.