Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yaonya kukabiliana na meli za adui
Jeshi la serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya limetangaza kuwa, liko tayari kukabiliana na meli yoyote ya adui itakayoingia katika maji ya Libya.
Jeshi la Libya limesisitiza kuwa vikosi vya nchi kavu na vya majini vya serikali ya mwafaka ya nchi hiyo viko tayari kukabiliana na adui; na kuonya kuwa litaishambulia meli yoyote ya adui itakayojaribu kuingia katika maji ya nchi hiyo.
Wakati huo huo kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la kitaifa la Libya lenye mfungamano na wanamgambo wa Khalifa Haftar mashariki mwa nchi hiyo kimeitungua ndege moja ya ujasusi isiyo na rubani ya Uturuki (droni) huko magharibi mwa mji wa Sirte.
Libya imetumbukia katika mapigano na mgogoro wa kisiasa kutokana na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo. Libya ina serikali mbili; moja ikiwa ile yenye makao makuu yake huko Tripoli mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sarraj na inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa. Aidha serikali yenye makao makuu yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi inaungwa mkono na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.