Spika wa zamani wa Bunge la Sudan atiwa nguvuni
-
Ibrahim Ahmed Omer
Askari usalama wa Sudan wamemtia nguvuni spika wa zamani wa Bunge la nchi hiyo.
Ibrahim Ahmed Omer ametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano ya kupinga marekebisho ya sheria za nchi yaliyofanyika hivi karibuni nchini humo.
Spika huyo wa zamani wa Bunge la Sudan alipinga hatua ya serikali ya mpito ya kuvunja chama cha Kongresi ya Kitaifa na kuzuia shughuli zake zote za kisiasa.
Aprili mwaka jana askari usalama wa Sudan pia walimtia nguvuni Ibrahim Ahmed Omer baada tu ya kurejea nchini akitokea Qatar na kumuweka katika kifungo cha nyumbani katika mji wa Omdurman.
Ijumaa iliyopita mamia ya Wasudani walifanya maandamano wakipinga marekebisho ya sheria za nchi yaliyofanywa na Serikali ya Mpito ya nchi hiyo na kupiga nara zinazoipinga serikali hiyo.
Waandamanaji hao wametoa wito wa kuondolewa madarakani serikali ya sasa ya Sudan.
Waandamanaji hao pia wametaka kutekelezwa sheria za dini, kufutwa marekebisho yaliyofanywa na Serikali ya Mpito kuhusiana na sheria za murtadi, kuhalalisha pombe kwa wasio Waislamu nchini Sudan na ukahaba na kuboreshwa hali ya maisha ya wananchi.
Wasudani wanasema marekebisho ya sheria yaliyofanywa na serikali ya sasa ya Khartoum yanapingana na mafundisho ya Uislamu na yanakwenda sambamba na matakwa ya wasekulari.