Spika wa Bunge la Tunisia aponea chupuchupu kuuzuliwa
Spika wa Bunge la Tunisia ameponea chupuchupu kupigiwa kura ya kutokuwa imani naye baada ya wabunge wanaompinga kushindwa kutimiza idadi ya kura 107 zilizohitajika ili kuweza kumuuzulu wadhifa huo.
Wabunge 97 wa bunge la Tunisia jana Alkhamisi walipiga kura dhidi ya Rashid al-Ghanushi, kinara wa chama cha Kiislamu chenye mielekeo ya wastani cha An-Nahdhah na kukosa kura 12 zilizohitajika ili kuweza kumvua wadhifa huo wa uspika.
Hata hivyo ushindi huo mwembamba aliopata Ghanushi unaweza kuzidisha migawanyiko ya kisiasa iliyoikumba Tunisia baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo kujiuzulu.
Baada ya chama chake cha An-Nahdhah na kile cha Karama kususia kupiga kura ili kuonyesha upinzani wao kwa hoja iliyowasilishwa bungeni ya kumuuzulu Al-Ghanushi, ni wabunge 16 tu wengine walioshiriki kwenye zoezi la upigaji kura waliomuunga mkono Spika huyo wa bunge la Tunisia.
Ushindi mwembamba aliopata Rashid al-Ghanushi unamaanisha kuwa chama cha An-Nahdhah sasa kitakabiliana na upinzani mkali bungeni wa vyama vilivyopiga kura dhidi yake na hivyo kutatiza juhudi za kutafuta mwafaka juu ya uundaji wa serikali mpya.
Upigaji kura wa kutaka kumng'oa Al-Ghanushi kwenye kiti cha uspika umefanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu serikali ya Tunisia ya waziri mkuu Elyes Fakhfakh ilipovunjka, ukiwa umepita muda wa chini ya miezi mitano tangu ilipoundwa.
Rais Kais Saied wa Tunisia alimteua waziri wa mambo ya ndani Hichem Mechichi kuwa waziri mkuu mpya, ambaye anapaswa kuunda serikali mpya itakayohitaji uungaji mkono mkubwa katika bunge la nchi hiyo lililogawanyika.../