Sudan yakataa kurejea katika mazungumzo kuhusu mzozo wa Bwawa la al-Nahdha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62719-sudan_yakataa_kurejea_katika_mazungumzo_kuhusu_mzozo_wa_bwawa_la_al_nahdha
Serikali ya Sudan imetangaza kukataa kurejea katika meza ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Bwawa la al-Nahdha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 10, 2020 00:08 UTC
  • Sudan yakataa kurejea katika mazungumzo kuhusu mzozo wa Bwawa la al-Nahdha

Serikali ya Sudan imetangaza kukataa kurejea katika meza ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Bwawa la al-Nahdha.

Viongozi wa Sudan wametangaza kuwa, nchi hiyo haiko tayari kurejea katika mazungumzo hayo katika mazingira ya hivi sasa.

Taarifa ya Sudan imeeleza kuwa, licha ya Ethiopia kutangaza kuendelea mazungumzo kuhusu Bwawa la al-Nahdha kuanzia Jumatatu ya leo, lakini Khartoum haiko tayari kurejea katika mazungumzo hayo.

Sudan imesisitiza kuwa, itarejea katika mazungumzo hayo pale Ethiopia itakapofungamana na makubaliano yaliyofikiwa hapo kabla.

Wakati huo huo, serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, haiko tayari kutia saini makubaliano ambayo yanaainisha hisa maalumu kwa nchi za Ukanda wa Mto Nile.

Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha ambao umezua hitilafu baina ya Ethiopia, Misri na Sudan

Hayo yanajiri katika hali ambayo, jana Ali Abdul-Aal, Spika wa Bunge la Misri alieleza kusikitishwa kwake na msimamo wa serikali ya Ethiopia aliutaja kuwa ‘usio wa ushirikiano’ kuhusiana na kadhia ya Bwawa la al-Nahdha.

Ujenzi wa Bwawa la  Renaissance (al-Nahdha) unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo mazuri na ya kuridhisha.