Waziri Mkuu mteule wa Tunisia: Nitaunda serikali ya mateknokrati watupu
-
Hichem Mechichi
Waziri Mkuu mteule wa Tunisia amesema kuwa ataunda serikali ya mateknokrati watupu bila ya kuvishirikisha vyama vingine kufuatia mivutano iliyopo baina vyama vya siasa kuhusu uundaji wa serikali mpya nchini humo.
Uamuzi huo wa Hichem Mechichi Waziri Mkuu Mteule wa Tunisia unatazamiwa kumtumbukiza kwenye dimbwi la mvutano na chama cha Kiislamu chenye misimamo ya wastani cha An Nahdhah. Chama hicho ambacho ni chama kikubwa cha kisiasa katika bunge la Tunisia kimetangaza kitapinga kuundwa serikali isiyo ya kisiasa nchini humo.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, pendekezo hilo la kuunda serikali ya mateknokrati watupu huko Tunisia bila ya kuvijumuisha vyama vya kisiasa litaungwa mkono na na Muungano Mkubwa wa Kibiashara wa nchi hiyo (UGTT) na vyama vingine vikiwemo Tahya Tounes na Dustoury el Hor.
Waziri Mkuu Mteule wa Tunisia amesema kuwa serikali atakayoiunda itajikita hasa katika tatizo la ugumu wa maisha na uchumi dhaifu wa nchi. Amesema, baadhi ya wananchi wa Tunisia hawana hata maji ya kunywa huku mivutano ya kisiasa ikiendelea kuigubika nchi hiyo.
Tunisia mwaka huu ilikumbwa na maandamano ya wananchi wakilalamikia ukosefu wa ajira, kukosekana maendeleo nchini na huduma mbovu za zafya, umeme na maji.