Jumuiya ya Maulamaa Algeria: Kuanzisha uhusiano na Israel ni haramu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62869-jumuiya_ya_maulamaa_algeria_kuanzisha_uhusiano_na_israel_ni_haramu
Jumuiya ya Maulamaa wa Algeria imesema, ni haramu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Aug 17, 2020 08:49 UTC
  • Jumuiya ya Maulamaa Algeria: Kuanzisha uhusiano na Israel ni haramu

Jumuiya ya Maulamaa wa Algeria imesema, ni haramu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel.

Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Imarati na Israel ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia baina yao, Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu wa Algeria, ambayo ni jumuiya kubwa zaidi ya maulamaa wa nchi hiyo imetoa taarifa ikisisitiza kuwa, kushirikiana na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu na vamizi ambao umeighusubu ardhi ya Palestina na kukanyaga matukufu yake ukiwemo msikiti wa Al Aqsa pamoja na watu wake ni uhaini na usaliti mkubwa ambao hauwezi kunyamaziwa.

Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu wa Algeria imesisitiza kuwa haijuzu kisharia kuitoa hata shubiri moja ya ardhi ya Palestina kwa sababu Palestina na Quds ni haki ya Wapalestina na Waislamu wote kwa ujumla na hakuna mtawala yeyote mwenye haki ya kuigawa ardhi hiyo.

Baadhi ya vyama vya siasa nchini Algeria, navyo pia vimelaani vikali makubaliano yaliyofikiwa kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni na kuyaelezea makubaliano hayo kuwa ni sawa kuwasaliti na kuwachoma jambia kwa nyuma wananchi wa Palestina.

Alkhamisi iliyopita, Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Imarati zilitoa taarifa ya pamoja zikitangaza kuwa, Abu Dhabi na Tel Aviv zinaanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia baina yao.

Makubaliano hayo yamepingwa na kulaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.../