Bunge la Tunisia lapasisha baraza jipya la mawaziri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63189-bunge_la_tunisia_lapasisha_baraza_jipya_la_mawaziri
Baada ya karibu mwezi mmoja tangu Rais Kais Saied alipomteuwa Hisham El-Mechishi kuwa Waziri Mkuu wa Tunisia, El-Mechishi amewasilisha baraza lake la mawaziri bungeni ambalo limepasishwa kwa wingi wa kura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 02, 2020 23:40 UTC
  • Bunge la Tunisia lapasisha baraza jipya la mawaziri

Baada ya karibu mwezi mmoja tangu Rais Kais Saied alipomteuwa Hisham El-Mechishi kuwa Waziri Mkuu wa Tunisia, El-Mechishi amewasilisha baraza lake la mawaziri bungeni ambalo limepasishwa kwa wingi wa kura.

Serikali ya El-Mechishi ina mawaziri 25 wakiwemo baadhi ya mawaziri wa serikali iliyopita. Serikali mpya ya Tunisia ina mawaziri 8 wanawake.

Hisham El-Mechishi ni waziri wa nne wa mambo ya ndani wa Tunisia ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali mpya baada ya mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zainul Abidin bin Ali. 

Inaonekana kuwa Tunisia imeingia katika awamu na kipindi kipya cha kisiasa. Ukweli ni kwamba, vyama mbalimbali vya siasa vya Tunisia vimeelewa vyema kipindi nyeti cha sasa na hatari kubwa inayoikabili nchi hiyo na kuamua kupasisha kwa kura nyingi serikali ya Hisham El-Mechishi. Awali chama cha Al Nahda chenye idadi kubwa ya viti vya Bunge la Tunisia kilikua kikisuasua katika kupasisha mawaziri waliopendekezwa na Hisham El-Mechishi. Idadi kubwa ya mawaziri waliopendekezwa na Waziri Mkuu wa Tunisia ni watu wasio na mfungamano wowote na vyama vya siasa kwa kadiri kwamba, baraza jipya la mawaziri nchini Tunisia linatajwa kuwa ni la serikali ya kiteknokrati (technocrat). Suala hilo limewafanya baadhi ya wanasiasa wachukue misimamo tofauti kuhusu baraza la mawaziri la Tunisia. Baadhi wanasema kuwa ndiyo inayofaa katika mgogoro wa sasa wa nchi hiyo, huku wengine wakihoji kuhusu "uteknokrati" wa serikali hiyo.

Rais Kais Saied (kulia) na Hisham El-Mechishi 

Khalil Al Baroumi ambaye ni mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya chama cha la Al Nahda amesema serikali ya El-Mechishi ni ya kiteknokrati na haina mfungamana na vyama vya siasa na kusema: Kimsingi chama cha Al Nahda kinapinga serikali ya kiteknokrati na isiyokuwa ya chama, na kinaunga mkono serikali inayotokana na chama na makundi ya kisiasa. Kwa sababu hiyo tangu El-Mechishi alipopewa jukumu la kuunda serikali mpya Al Nahda imejikuta katika hali ngumu; hata hivyo itashirikiana na serikali yake. 

Waungaji mkono wa serikali isiyotokana na chama wanaamini kuwa, mivutano ya kisiasa nchini Tunisia ni miongoni mwa sababu za hali inayoshuhudiwa nchini humo na kwamba matatizo ya sasa ya Tunisia yamewafanya wananchi wakose imani na wanasiasa. Katika upande mwingine hitilafu za kisiasa baina ya vyama tofauti vya Tunisia zimeshadidi zaidi na kuzuia kabisa uwezekano wa kushirikiana na kuungana kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi. Katika uwanja huo Waziri Mkuu mpya wa Tunisia anasema: Hitilafu baina ya vyama vya siasa zimekuwa kubwa zaidi na sasa nimefikia uamuzi kwamba, haiwezekani kuunda serikali itayojumuisha vyama vya siasa nchini Tunisia.  

Hisham El-Mechishi 

Takwimu zinaonesha kuwa, kiwango cha ustawi wa kiuchumi mwaka 2020 nchini Tunisia kitapungua kwa asilimia 6.1 na kiwango cha ukosefu wa ajira na kazi kitaongezeka kwa asilimia 19. 
Mazingira haya ya kisiasa yanayotawala Tunisia yamezidisha uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kadiri kwamba, wataalamu na maafisa wengi wa nchi hiyo wanatahadharisha kuhusiana na suala hilo.
Mshauri wa zamani wa serikali ya Tunisia, Jouhar bin Mubarak ametilia mkazo udharura wa kuchukuliwa msimamo imara wa kisiasa na kidiplomasia dhidi ya nchi zinazoharibu na kuvuruga hali ya ndani ya Tunisia zikiongozwa na Saudi Arabia na Imarati na amemtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo kukomesha njama za nchi hizo za kutaka kuzusha vurugu na machafuko nchini Tunisia na kuwaruhusu wananchi watatue matatizo ya nchi yao. 
Alaa kulli hal, Watunisia wana matumaini kwamba, serikali mpya ya nchi hiyo itachukua maamuzi muhimu ya kuboresha hali ya kiuchumi na kisiasa. Watunisia wengi pia wanatarajia kwamba, Waziri Mkuu Hisham El-Mechishi atalipa kipaumbele suala la kutayarisha nafasi za ajira na kupambana na ufisadi.