Mwakilishi wa kudumu wa Tunisia UN afutwa kazi ghafla
Mwakilishi wa kudumu wa Tunisia katika Umoja wa Mataifa ambaye hajatimiza hata miezi sita tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo, amefutwa kazi ghafla tena bila ya kupewa taarifa mapema.
Gazeti la al Swabah la Tunisia limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imejaribu kupunguza makali ya hatua hiyo kupitia taarifa yake maalumu na kusema kuwa, hatua ya kumrudisha nyumbani Qeis Qabtani ni sehemu ya mabadiliko ya kila mwaka ya wakuu wa vituo mbalimbali vya kidiplomasia na balozi kubwa na ndogo za Tunisia nje ya nchi hiyo na kwamba Qabtani atapangiwa sehemu nyingine ya kazi.
Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje wa Tunisia imesema, kubadilishwa wawakilishi wa kudumu wa nchi hiyo huko UN hakuleti taathira yoyote hasi katika siasa za mambo ya nje za Tunis.
Hata hivyo, Qeis Qabtani mwenyewe ameamua kujiuzulu rasmi nafasi zake zote za kidiplomasia ikiwa ni kuonesha kupinga hatua iliyochukuliwa dhidi yake na tena bila ya kupewa taarifa mapema.
Qabtani amesema, katika kipindi hicho kifupi cha kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tunisia huko Umoja wa Mataifa, amefanya juhudi zake zote kuhakikisha anatekeleza inavyopasa kazi zake, lakini hatua hiyo ya serikali ya Tunis imemvunja moyo sana na hana imani tena na Rais Kais Saied.
Vile vile amesema, wapambe wa rais huyo ndiyo sababu kubwa iliyopelekea afutwe kazi ghafla na bila ya kupewa taarifa mapema.
Amesema tangu Tunisia ipate uhuru hadi hivi sasa, hii ni mara ya kwanza kwa mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa kufutwa kazi bila ya kupewa taarifa mapema.